TANGAZO
ASKARI WA JWTZ,POLISI NA MAGEREZA WAKIWA KWENYE HARAKATI ZA KUPANGA MIFUKO YA MCHANGA NA MAWE KWENYE KINGO ZA KIWANDA HICHO CHA KUCHAKATA GESI ASILIA MSIMBATI MKOANI MTWARA. |
Na Clarence Chilumba, Mtwara.
Serikali mkoani Mtwara imeanza kuchukua hatua za awali
za kunusuru kiwanda cha kuchakata gesi asilia kilichoko eneo la Msimbati mkoani
humo ili kisiendelee kuharibiwa kwa maji ya bahari yanayoendelea kuingia ndani
ya kiwanda hicho
Moja ya jitihada hizo ni zile za kupeleka zaidi ya
askari 300 wa jeshi la wananchi Tanzania (JWTZ) katika eneo hilo kwa lengo la
kukinusuru kiwanda hicho kisifungwe kufuatia mvua kubwa zinazoendelea kunyesha
mkoani humo.
Aidha vikosi hivyo vimepelekwa kwenye eneo hilo la
kiwanda kwa kazi ya kupanga mawe na mchanga kwenye kingo za kiwanda hicho ili
kuzuia maji ya bahari yasiendelee kujaa na kuingia ndani ya eneo hilo la
kiwanda kinachoelekea kuharibika.
Hatua hiyo ya serikali mkoani Mtwara imekuja mara
baada ya kutokea kwa mtikisiko wa ardhi pamoja na upepo mkali ukiambatana na
mawimbi makubwa ya bahari kuvuma na kusababisha mmomonyoko wa ardhi uliokuwa
unaelekeza maji ya bahari kuingia ndani ya kiwanda hicho.
Jitihada hizo za serikali mkoani mtwara zimekuwa zikifanywa
kwa kasi zaidi ili kuepuka kiwanda hicho kisifungwe kwani
kufungwa kwa kiwanda hicho kutapelekea wakazi wa mikoa ya lindi na mtwara
kukosa umeme kwa zaidi ya miezi sita.
Akiongea na waandishi wa habari katika eneo la kiwanda
hicho kaimu mkuu wa mkoa wa mtwara
ambaye pia ni mkuu wa wilaya ya Tandahimba Ponsiano nyami alisema jitihada hizo zimeanza mara baada ya kikao cha
kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa wa Mtwara kukaa na kuazimia hatua za awali
zichukuliwe.
Alisema wananchi mkoani Mtwara wanapaswa kuwa watulivu
katika kipindi hiki huku wakiombwa kuunga jitihada zinzofanywa na serikali ya
mkoa ili kunusuru adha inayoweza kujitokeza ya wakazi wa mkoa huo kukosa umeme
kwa zaidi ya miezi sita endapo kiwanda hicho kitafungwa.
LORI LILILOBEBA MAWE LIKISHUSHA MAWE HAYO KIWANDANI HAPO HUKU VIKOSI HIVYO YA JESHI VIKISUBIRI KWA AJILI YA KUWEKA KWENYE MIFUKO.
Kwa Upande wake mhandisi wa kiwanda hicho Peter John
alisema hali hiyo imetokana na
ongezeko la kina cha maji ya bahari na kusababisha mawimbi makubwa yanayotishia
kumeza mitambo hiyo kufuatia mmomonyoko wa ardhi mita 24 kutoka usawa wa bahari
hadi eneo la mitambo hiyo.
Alisema iwapo
hali hiyo haitadhibitiwa kwa wakati watalazimika kufunga kiwanda hicho na
kusababisha mikoa ya Lindi na Mtwara kuwa gizani kwa muda wa zaidi ya miezi sita mfululizo.
UKINGO ULIOPO KUZUNGUKA KIWANDA HICHO UKIWA UMEHARIBIKA VIBAYA KUTOKANA NA MVUA KUBWA ZINAZOENDELEA KUNYESHA MKOANI MTWARA.
Naye kamanda wa kikosi maalumu cha jeshi la wananchi
wa Tanzania (JWTZ) Luteni kanali Idi saidi kambi alisema kuwa jitihada
za kunusuru kiwanda hicho zinaendelea vizuri na kwamba tayari zaidi ya
wanajeshi 300 wako eneo la kiwanda wakishiriki zoezi hilo ambapo pia wamo
vikosi vya jeshi la polisi na magereza.
ASKARI WA JWTZ,MAGEREZA PAMOJA NA POLISI MKOANI MTWARA WAKIWA KWENYE HEKAHEKA ZA KUKINUSURU KIWANDA CHA KUCHAKATA GESI ASILIA MKOANI MTWARA HUKO MSIMBATI
Kwa upande wa shirika la petroli nchini TPDC kupitia
kwa mkurugenzi wa shirika hilo hapa nchini James Mataragio alisema tatizo hilo linatokana na mvua kubwa zinazoendelea
kunyesha nchi jirani za Msumbiji na
Malawi.
Alisema shirika la petroli nchini linatarajia kupokea
wataalamu hivi karibuni kutoka nje ya nchi watakaoshiriki katika kunusuru hali
iliyopo kwa sasa kwenye kiwanda hicho cha kuchakata gesi asilia.
Mwisho.
HIVI NDIVYO HALI ILIVYOKUWA KATIKA ENEO LA MSIMBATI NA KWAMBA ENDAPO VIKOSI HIVYO VITASHINDWA KUZUIA HALI HIYO BASI WAKAZI WA MIKOA YA LINDI NA MTWARA WATAKUWA GIZANI KWA ZAIDIYA MIEZI SITA (6) MFULULIZO.
HONGERA VIKOSI VYA MAJESHI MKOANI MTWARA PAMOJA NA SERIKALI YA MKOA KWA UJUMLA KWA KULIONA HILI MAPEMA.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD