TANGAZO
DC
MASASI AWAPONGEZA REA
Na
Clarence Chilumba, Masasi.
Mkuu wa wilaya ya
Masasi mkoani Mtwara Ajati Farida Mgomi amewapongeza wakala wa nishati vijijini
kwa programu yao ya mafunzo inayoendelea wilayani humo itakayosaidia
kukabiliana na uharibifu wa mazingira ya bahari.
Aidha mpango huo wa REA
una lengo la kuhakikisha kuwa malengo ya MKUKUTA ya kufikisha nishati bora na
yenye uhakika ya umeme kwa wananchi waishio vijijini inafanikiwa ifikapo mwaka
2015.
Hayo aliyasema juzi
wakati anafungua mafunzo ya siku tano ya ukaushaji wa samaki kwa kutumia
nishati ya jua yaliyoshirikisha washiriki 20 kutoka Somanga wilaya ya Kilwa
mkoani Lindi katika ukumbi wa chuo cha maendeleo ya wananchi mjini Masasi.
Alisema mafunzo hayo
yatachangia kuboresha shughuli za uvuvi kwenye maeneo ya bahari ya Hindi hivyo
kukuza soko la samaki na kuchangia maendeleo kwa jamii kwa lengo la kupungzua
umaskini wa kipato kwa wananchi.
Mgomi alisema matumizi
ya nishati ya jua katika ukaushaji samaki kutaboresha ubora wa samaki hao na
bidhaa zingine zitakazokaushwa kwa kutumia teknolojia hiyo ambapo ametoa wito
kwa washiriki hao kutumia fursa hiyo ya mafunzo kikamilifu.
Alisema hatua ya wakala
wa nishati vijijini ya kuandaa mafunzo hayo ya matumizi ya nishati ya jua
italisaidia taifa kuondokana na uharibifu wa mazingira unaotokana na ukataji
miti katika ukaushaji wa mazao kama vile ya samaki, matunda pamoja na
mbogamboga.
Wakizungumza kwa niaba
ya washiriki wa mafunzo hayo Yusuph
Kitelebu ambaye ni msimamizi wa rasilimali za bahari (BMU) pamoja na Hamida
Mjanaeli ambaye ni mhitimu wa shahada katika chuo cha ustawi wa jamii Dar es
salaam walisema kuwa matarajio yao katika mafunzo hayo ni kupata elimu ya
ukaushaji samaki kwa kutumia nishati ya jua.
Walisema kuwa
changamoto kubwa iliyopo kwa wananchi wengi hapa nchini ni kuona kuwa
rasilimali zilizopo ni zawadi kutoka kwa mungu mazingira yanayopelekea wengi
wao kutolinda na kutunza rasilimali hizo.
Kwa upande wake mkuu wa
chuo cha maendeleo ya wananchi Masasi ambaye pia ndiye mwezeshaji wa mafunzo
hayo Fred Mwakagenda alisema ukaushaji wa samaki kwa kutumia nishati ya jua ni
njia muafaka ya kuboresha mazao ya samaki hapa nchini.
Mwisho.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD