Loading...
ADVERTISE WITH US ON THIS BLOG.CALL +255 714 789 592/ +255 682 997 767/ +255 752 944 022

MILIONI 50 ZA KILA KIJIJI ZILIZOAHIDIWA NA DK.MAGUFULI ZAIVA,LINDI NA MTWARA KUPEWA KIPAOMBELE

TANGAZO
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.John Magufuli (picha ya Maktaba)

Hatimaye serikali imetengua kitendawili cha lini ahadi ya Rais John Magufuli ya kutoa Sh. milioni 50 za maendeleo kwa kila kijiji nchini itatekelezwa, kama alivyoahidi wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu mwaka jana. 

Aidha, katika mpango wa utekelezaji wa ahadi hiyo, serikali imetenga Sh. bilioni 811 na imeshaanza kushirikisha wadau mbalimbali ili kupata maoni ya kuendesha mchakato huo kwa ufanisi na tija. 

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam baada ya kikao cha wadau waliokuwa wakijadili rasimu ya mpango huo mwishoni mwa wiki, Katibu Mtendaji wa Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), Beng'i Issa, alisema serikali itaanza kutoa fedha hizo kuanzia mwaka ujao wa fedha.

"Kwa kuanzia, fedha  hizo zitatolewa kwa awamu tatu katika kipindi cha miaka mitano,” alisema na kuongeza:  
"Fedha hizo zitatolewa benki kabla ya kutolewa kwa vikundi mbalimbali kama Vicoba na Saccos kulingana na taratibu zitakazowekwa."

Kwa mujibu wa mpango huo, mchakato utaanza na mikoa 10 nchini iliyo nyuma katika kutumia huduma za kifedha. Mikoa hiyo, kwa mujibu wa taarifa ya utafiti ya Finscope ya mwaka 2013 ni  Singida, Lindi, Mtwara, Mbeya, Shinyanga, Geita, Kagera, Dodoma, Rukwa na Ruvuma. 

Akifungua mkutano huo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Walemavu, Jenista Mhagama, alisema mkutano huo ulilenga kupata maoni ya wataalamu namna bora ya kutekeleza mpango huo.

Akizungumza kwa niaba ya waziri, Kaimu Mkurugenzi, Maendeleo ya Sekta Binafsi, Uwekezaji na Uwezeshaji, Ofisi ya Waziri Mkuu, Victor Mwainyekule, alisema mawazo yaliyopatikana yatazingatiwa ili kuboresha kazi hiyo, yenye lengo la kupambana na umasikini.

Kwa upande wake, Mkuu wa Uendeshaji wa Benki ya Wanawake (TWB), Zablon Yebete, alisema mpango huo ni uwekezaji mkubwa kwa Watanzania unaopaswa kuungwa mkono na vyombo vya fedha na wadau wengine nchini.

Kwa mujibu wa mpango huo, walengwa watapatiwa mafunzo ya ujasiriamali kabla ya kupatiwa fedha.

Mkutano huo ulihudhuriwa na wawakilishi wa halmashauri za wilaya, Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf), benki, mifuko ya hifadhi ya jamii na vikundi mbalimbali.

TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD
Newer Posts Older Posts
© Copyright Mtazamo Mpya | Designed By FAHARI YA TANZANIA
Back To Top