TANGAZO
Katibu Tawala wa wilaya ya Masasi Danford Peter akizungumza wakati wa ufunguzi wa semina kwa wachimbaji wadogo wa madini,wenyeviti wa vijiji,watendaji wa vijiji,kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya pamoja na wakuu wa idara Halmashauri ya wilaya ya Masasi hii leo kwenye ukumbi wa Emirates Mjini Masasi.
Na Clarence
Chilumba,Masasi.
WATENDAJI wa serikali
pamoja na wachimbaji wadogo wa madini nchini wametakiwa kuwa na uelewa kuhusu
sheria ya madini ili waweze kusaidia katika kusimamia sheria hiyo na kwamba wanapaswa
kuhakikisha kuwa katika maeneo yao shughuli za utafutaji,uchimbaji na biashara
ya madini vinafanyika kwa mujibu wa sheria za nchi.
Hayo yalisemwa jana
na katibu tawala wa wilaya ya Masasi Danford Peter wakati anafungua semina kwa
wenyeviti wa vijiji,watendaji wa vijiji,wachimbaji wadogo pamoja na baadhi wa
wakuu wa idara wa Halmashauri ya wilaya ya Masasi ambapo alisema watendaji wa
serikali wanapaswa kusimamia uvamizi wa maeneo yenye leseni halali za uchimbaji
madini.
Alisema kifungu cha 6
cha sheria ya madini ya mwaka 2010 pamoja na kanuni zake zilizoanza kutumika Novemba ,2010 imeeleza
wazi mamlaka pekee ya usimamizi wa shughuli za madini kuwa ni wizara ya nishati
na madini na kwamba kufanya utafiti,uchimbaji,biashara pamoja na uchenjuaji
bila kibali au leseni kutoka kwa mamlaka hiyo ni kosa.
Alisema viongozi
katika ngazi ya halmashauri wanapaswa kusaidia katika kuhamasisha wachimbaji
wadogo wa madini kulipia ada na tozo mbalimbali ikiwemo mrabaha,ada za mwaka za
leseni na tozo kwa Halmashauri husika lengo likiwa ni kuzifanya halmashauri
nchini kunufaika na sekta ya madini kwa kujiongezea kipato na kupunguza utegemezi wa
ruzuku kutoka serikali kuu.
Kwa mujibu wa katibu
tawala wa wilaya ya Masasi alisema shughuli za uchimbaji wa madini hufanyika
kwenye maeneo ya vijiji hivyo ni vyema watendaji wa serikali wa ngazi hizo
wakafahamu vizuri sera,sheria na kanuni zinazosimamia uchimbaji na biashara ya
madini ili kuepusha migongano ya kimaslahi ambayo imekuwa ikitokea katika
maeneo mengi yanayochimbwa madini nchini.
Aidha alitoa rai kwa
wachimbaji wadogo wa madini nchini kuwa mabalozi wazuri katika kufikisha ujumbe
wa maelekezo ya serikali yanayotolewa kwenye mafunzo hayo na kwamba wafanye
shughuli zao za uchimbaji kwa kufuata sheria ya madini na kanuni zake.
Alisema wachimbaji wadogo
ni kundi ambalo limekuwa likilalamika kila siku kuwa linatengwa na viongozi wa
serikali na kwamba jambo hilo halina ukweli wowote tatizo lililopo ni kwa
baadhi ya wachimbaji hao kushindwa kufuata kanuni na sheria ya madini ambapo
aliwahimiza pia kuwa mstari wa mbele katika kulipa kodi,mrabaha
na tozo mbalimbali.
Kamishna msaidizi wa madini kanda ya kusini,Injinia Benjamin Mchwampaka akizungumza wakati wa kumkaribisha katibu tawala wa wilaya ya Masasi Danford Peter (Kushoto kwake) ili aweze kuzungumza na washiriki wa semina hiyo kwenye ukumbi wa Emirates.
Kwa upande wake
kamishna msaidizi wa madini kanda ya kusini Injinia Benjamin Mchwampaka alisema
watendaji wa vijiji ambapo madini hupatikana wawapokee vizuri wawekezaji wanaokuja kufanya tafiti
mbalimbali za madini kwenye maeneo yao huku akiwaonya kuacha kuwasumbua kwa kuwadai
vibali kwa kuwa mwenye mamlaka ya kutoa kibali kwa mchimbaji au mtafiti ni
waziri mwenye dhamana,kamishna wa madini pamoja na ofisa madini wa kanda.
Alisema wenyeviti wa
vijiji pamoja na watendaji wao watumie lugha nzuri kwa wawekezaji hao na kwamba
si kweli kwamba mwekezaji anapokuja kufanya utafiti anapaswa kulipa ushuru kwa
serikali ya kijiji ambapo ukweli ni kwamba makubaliano kati ya mwekezaji na
serikali ya kijiji husika hufanywa wakati wa uchimbaji wa madini kuona ni kwa
namna gani jamii inayozunguka eneo la mgodi litanufaika.
BAADHI ya washiriki wa semina hiyo wakifuatilia kwa karibu hotuba ya mgeni rasmi (hayuko pichani) ambaye alikuwa ni katibu tawala wa wilaya ya Masasi Danford Peter.
Wakizungumza nje ya
ukumbi wa mkutano huo baadhi ya washiriki wa semina hiyo walisema kitendo
kilichofanywa na wizara ya nishati na madini kwa kushirikiana na ofisi ya
madini kanda ya kusini kutoa mafunzo hayo kitaleta mabadiliko makubwa katika
sekta hiyo kwa kuzingatia kuwa baadhi ya kanuni zilizopo kwenye sheria ya
madini ya mwaka 2010 zilikuwa hazifahamiki kwao.
WADAU wa Sekta ya madini nchini wakiwa kwenye picha ya pamoja na katibu tawala wa wilaya ya Masasi Danford Peter (wa pili kutoka kulia waliokaa),kulia kwake ni Injinia Benjamin Mchwampaka,kamishna msaidizi wa madini kanda ya kusini nje ya ukumbi wa semina wa Emirates Mjini Masasi.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD