TANGAZO
Gari ndogo aina ya Toyota Escudo lenye namba za usajili T 872 AUP lililokuwa likiendeshwa na askari wa jeshi la polisi Tanzania wilaya ya Masasi marehemu PC Twalibu likiwa limeegeshwa kituo cha polisi Masasi.
Na Clarence
Chilumba: Masasi.
Watu wawili akiwemo
askari wa jeshi la polisi Tanzania wilaya ya Masasi wamefariki dunia papo hapo
huku wengine wawili wakipata majeraha kwa ajali iliyohusisha magari matatu iliyotokea
huko katika kijiji cha Mailisita Halmashauri ya mji wa Masasi mkoani Mtwara.
Tukio hilo lililoacha
simanzi kwa jeshi la polisi mkoa wa Mtwara pamoja na wananchi kwa ujumla
lilitokea jana majira ya saa 1:00 usiku katika kijiji cha Mailisita Halmashauri
ya mji wa Masasi kwa kuhusisha magari matatu likiwemo la watu waliofariki
dunia.
Magari matatu
yaliyohusika kwenye ajali hiyo ni lori aina ya Jiefang lenye namba za usajili T
193 ACH lililokuwa likiendeshwa na dereva Kassimu Mohamedi (28) mkazi wa
Masasi,gari ndogo aina ya prado lenye namba za usajili T 263 BLE likiendeshwa
na Emanuel Mgeni mkazi wa Masasi pamoja na gari ndogo aina ya Toyota Escudo
lililokuwa likiendeshwa na marehemu Twalibu lenye namba za usajili T 872 AUP.
Gari lililopata ajali na kusababisha vifo vya watu wawili katika eneo la mailisita Halmashauri ya mji wa Masasi mkoani Mtwara.
Akithibitisha kutokea
kwa tukio hilo kamanda wa polisi mkoa wa Mtwara Henry Mwaibambe alisema ajali
hiyo imesababisha vifo vya watu wawili na kusababisha majeruhi makubwa kwa watu
wawili ambao wamelazwa katika hospitali ya misheni ya Ndanda huku wengine
wanane wakipata matibabu na kuruhusiwa kurudi nyumbani.
Mwaibambe aliwataja
waliofariki dunia kwenye ajali hiyo kuwa ni askari wa jeshi la polisi Tanzania
F.9006 PC Twalibu (35) mkazi wa mkoa wa Kigoma aliyeripoti kituo cha polisi wilaya ya Masasi jana hiyo hiyo akitokea katika kikosi cha
kutuliza ghasia mkoani Mtwara FFU ambapo baadae alielekea Ndanda kwa matembezi
ya kawaida na wakati anarejea Masasi alipata ajali na kufariki dunia papo hapo.
Alisema mwingine
aliyefariki kwenye ajali hiyo ni Sophia Shaibu mkazi wa kijiji cha Mailisita
Halmashauri ya mji wa Masasi inayedaiwa kuwa aliomba msaada wa usafiri kwa
marehemu kutoka Ndanda na kwamba kabla hawajafika eneo ambalo alitakiwa ashuke
ikatokea ajali hiyo na kufariki dunia.
Kwa mujibu wa kamanda
wa polisi mkoa wa Mtwara aliwataja waliojeruhiwa vibaya kuwa ni pamoja na Alex
Edward Msomi ambaye pia ni askari wa jeshi la polisi Tanzania wilaya ya Masasi aliyekuwa kwenye gari dogo aina ya Toyota
Escudo lenye namba za usajili T 872 AUP lililokuwa likiendeshwa na marehemu askari
mwenzake Twalibu.
Alisema mwingine
aliyejeruhiwa ni Emanuel Mgeni mkazi wa Masasi ambaye alikuwa dereva kwenye gari aina ya Prado lenye namba za usajili T
263 BLE aliyepata majeraha mwilini ambao wote kwa pamoja wamelazwa kwenye
Hospitali ya misheni ya Ndanda na hali zao zinaendelea vizuri.
Gari aina ya Prado ambalo nalo limepata ajali lakini hakuna aliyefariki dunia kwenye gari hiyo licha ya dereva wake kupata ajali na kulazwa katika hospitali ya misheni ya Ndanda.
Kamanda mwaibambe
alisema watu waliokuwepo kwenye lori hakuna aliyepata majeraha yoyote huku
akikiri kuwa kwenye gari aina ya Prado kulikuwa na watu tisa na kwamba
aliyepata majeraha ni dereva peke yake na wengine wakibaki salama ambao wote
walikuwa wanawake.
Alisema chanzo cha
ajali hiyo ni mwendo kasi wa dereva wa gari aina ya Prado aliyetaka kulipita
lori lililokuwa mbele yake ambapo alipojaribu kufanya hivyo aliligonga lori
hiyo upande wa tairi la kulia na kwa kuwa lilikuwa kwenye mwendo liligeuka na
kukutana uso kwa uso na gari ndogo aina ya Escudo na kusababisha vifo kwa watu
wawili waliokuwepo kwenye gari hiyo.
Aidha kamanda wa
jeshi la polisi mkoa wa Mtwara alisema kuwa upelelezi wa tukio hilo bado
unaendelea na miili ya marehemu ikiwa imehifadhiwa kwenye hospitali ya
Mkomaindo mjini Masasi ikisubiri taratibu zingine za mazishi huku akiwaomba madereva
wa vyombo vya moto kuzingatia kanuni za usalama barabarani.
Mwisho.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD