TANGAZO
![]() |
Mbunge wa Kigoma Kaskazini Zitto Kabwe. |
Dar es Salaam.
Pamoja na mpango
wa Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe kuliaga Bunge kukwama jana, Chama
cha ACT- Tanzania kimetangaza kukamilisha maandalizi ya kumpokea mwanasiasa
huyo kuanzia leo.
Mbunge huyo
alipanga kuliaga bunge na alisema amekwishapata ruksa ya Spika kuwa angesimama
bungeni kuwaaga wabunge na wanachama wa Chadema baada ya chama hicho kumtimua
uanachama wake hivi karibuni, lakini ghafla mpango huo uliyeyuka kwa kile
kilichoelezwa kuwa Spika amemkatalia.
Tangu kuanzishwa
kwa chama hicho mwaka mmoja uliopita, Zitto amekuwa akihusishwa kukianzisha,
hivyo kitendo chake cha kujiunga nacho kitahitimisha mjadala wa muda mrefu wa
mashabiki wake waliokuwa wakihoji wapi ataelekea baada ya kung’olewa Chadema.
Akizungumza na
gazeti hili jana, Katibu Mkuu wa ACT, Samsom Mgamba aliangua kicheko na bila
kuuma maneno alisema: “Hahahaa... tutampokea kuanzia kesho (leo) na maandalizi
yamekamilika.”
Alipotakiwa
kueleza wapi mapokezi hayo yatafanyika alisema: “Hilo mbona liko wazi,
yatafanyikia makoa makuu yetu (yapo Makumbusho, Dar es Salaam) lakini kwa
taarifa zaidi tutawajuza.”
Zitto anaingia
ACT ikiwa ni siku tisa kabla ya chama hicho kufanya uchaguzi wake mkuu, huku
akitajwa kuwa ameandaliwa kushika wadhifa wa mwenyekiti kuendeleza harakati
zake za siasa.
Hivi karibuni,
chama hicho kilimvua uongozi aliyekuwa mwenyekiti mwanzilishi, Lucas Limbu
kutokana na mgogoro uliokuwapo baina ya viongozi na kufanya nafasi hiyo kubaki
wazi.
Tayari washirika
wa Zitto waliohusishwa naye kuandika waraka wa mapinduzi ndani ya Chadema na
baadaye kufukuzwa uanachama, Mwigamba na Profesa Kitila Mkumbo wametua ndani ya
chama hicho kipya.
Chama hicho
ambacho kinaendelea na uchaguzi katika ngazi ya mikoa kikibakiza Mkoa wa Geita
unaofanya uchaguzi wake kesho. Kitaanza vikao vyake vya kitaifa Machi 27 na
kuhitimisha kwa mkutano mkuu Machi 29.
Akizungumzia
uchaguzi huo, Mwigamba alisema: “Maandalizi yanakwenda vizuri na hakuna shaka
utafanikiwa kwa kiasi kikubwa na tunawaomba Watanzania watuunge mkono.”
Tangu juzi, Zitto
alitarajiwa kuliaga Bunge lakini hakufanya hivyo kwa kilichoelezwa kuwa aliitwa
na Spika wa Bunge, Anne Makinda na kupewa ushauri kuwa afanye hivyo jana jioni.
Jana asubuhi
mbunge huyo hakuingia katika kikao cha Bunge lakini alionekana katika viwanja
vya Bunge akiwa amevaa shati la drafti na suruali ya kaki akizungumza na rafiki
yake wa karibu, Deo Filikunjombe ambaye ni mbunge wa Ludewa kupitia CCM.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD