TANGAZO
Na
Clarence Chilumba, Masasi.
Wazazi,
walezi pamoja na walimu wametajwa kuwa ni vinara katika matukio makubwa ya
ukatili na unyanyasaji dhidi ya watoto ambayo kwa mujibu wa takwimu yanaonesha
kuendelea kuongezeka mazingira ambayo husababisha watoto wengi kuishi katika
mazingira hatarishi.
Aidha
takwimu nchini zinaonesha kuwa kwa kila watoto kumi wa kike watoto watatu
walifanyiwa vitendo vya ukatili wa kingono huku kwa kila watoto saba wa kiume
mtoto mmoja kati yao alifanyiwa ukatili wa kingono.
Pia vitendo hivyo vimeelezwa
kuongezeka kwa kasi ambapo asilimia 72 ya ukatili wa kujeruhiwa kimwili
walifanyiwa watoto wa kike huku asilimia 71 ya vitendo hivyo vya kikatili
wakifanyiwa watoto wa kiume na kwamba vinara wa vitendo hivyo wakitajwa kuwa ni
wazazi pamoja na walimu.
Hayo yalisemwa jana na Ofisa
maendeleo ya jamii wa Halmashauri ya mji wa Masasi mkoani Mtwara Zuena Ungele
wakati akitoa taarifa ya timu ya ulinzi na usalama wa mtoto ya Halmashauri ya
mji wa Masasi kwenye maadhimisho ya wiki
ya ulinzi na usalama wa mtoto kwenye viwanja vya Terminal Two Mjini humo.
Alisema asilimia 60 ya watoto
waliofanyiwa vitendo vya kikatili vya kimwili walisema kuwa waliowafanyia ni
wazazi wao huku asilimia 50 ya vitendo hivyo vya kikatili wakibebeshwa lawama
na shutuma hizo walimu.
Kwa mujibu wa Ungele alisema kuwa
kutokana na kuongezeka kwa takwimu za watoto kulawitiwa, kubakwa, kufanyishwa
kazi ngumu pamoja na kupigwa serikali kwa kushirikiana na shirika lisilo la
kiserikali la terre des homes Netherlands la nchini Uholanzi lilianzisha timu
za ulinzi na usalama wa mtoto kwa kwa baadhi ya wilaya nchini ikiwemo Masasi
kwa lengo la kumlinda mtoto na vitendo vyote vya kikatili.
Alisema moja ya majukumu ya
kamati hizo kwa ngazi ya wilaya ni pamoja na kuijengea uelewa jamii juu ya
kupambana na ukatili wa aina yoyote, kutambua mahitaji ya watoto waliofanyiwa
vitendo hivyo pamoja na kusimamia kamati za ulinzi na usalama wa mtoto kwanye
ngazi ya kata.
Alisema katika kipindi chote
ambacho timu ya ulinzi na usalama ya mtoto imekuwa ikifanya kazi jumla ya
matukio ya kesi 11 ziko katika mahakama ya wilaya ya Masasi ikiwemo kesi ya
Baba wa miaka 52 kumlawiti mtoto wake wa kiume wa miaka (9), pamoja na kesi ya
babu wa miaka 44 kumlawiti mjukuu wake wa kike wa miaka 13.
Aidha tayari timu imefanikiwa
kuanzisha jumla ya klabu kumi za watoto wa shule za msingi Halmashauri ya mji
Masasi zitakazokuwa na jukumu la kufanya midahalo mbalimbali kuhusu athari ya
vitendo vya kikatili dhidi ya watoto.
Ofisa
maendeleo ya jamii huyo alizitaja changamoto ambazo hukwamisha utendaji kazi wa
timu ya ulinzi na usalama ya mtoto ikiwemo ufinyu wa bajeti,upungufu wa
vitendea kazi,kukosekana kwa usafiri kwa ajili ya ufuatiliaji wa matukio hayo
pale yanapojitokeza pamoja na baadhi ya wazazi kuwapa vitisho watoto wao pale
wanapohitaji kuripoti vitendo hivyo.
Mwisho.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD