TANGAZO
Bwana Jofrey Evance akiwa Wodini Mkomaindo. |
Wakazi watano wa familia
moja wa kitongoji cha Benaco kata ya mtandi Halmashauri ya mji wa Masasi mkoani
Mtwara wamelazwa katika hospitali ya Mkomaindo huku hali zao zikiwa mbaya baada
ya kunywa dawa ya kienyeji waliyopewa na mganga wa tiba za asili.
Dawa hiyo ya kienyeji
waliyopewa na mganga huyo inaitwa Nyungu ambayo hutokana na mchanganyiko wa
majani tofauti ambayo hupondwa kwenye kinu na kuchanganywa na maji na
kuchemshwa na kwamba mgonjwa hufunikwa kwa nguo nyeupe na kuvukizwa na mvuke wa
maji hayo kasha mgonjwa hunywa maji hayo.
Aidha katika hali ya
kushangaza baada ya wanafamilia hao kunywa dawa hiyo wote hali zao zilibadilika
ghafla wanafamilia hao walianza kuweweseka wasijue wananchokifanya huku
wakitokwa na mapovu meupe kinywani na
baadae walipoteza fahamu na kukimbizwa katika hospitali ya Mkomaindo ambako
wamelazwa hadi sasa.
Kwa mujibu wa mkuu wa
jeshi la polisi wilaya ya Masasi Azaria Makubi alithibitisha kutokea kwa tukio
hilo na kusema kuwa tukio hilo lilitokea jana majira ya saa 12:30 jioni katika
eneo la Makondeko Halmashauri ya mji wa Masasi nyumbani kwa mganga huyo.
Alisema wana familia hao
walikumbwa na kadhia hiyo mara baada ya kuitwa na mganga huyo msichana mwenye
umri wa miaka 17 aliyetambulika kwa jina moja tu la Emele kwa lengo la kwenda
kumalizia dawa hiyo ya kinga kwa wanafamilia hao kufuatia watoto wao wawili
kupewa matibabu na mganga huyo wiki mbili zilizopita.
Makubi aliwataja wanafamilia
ambao hali zao ni mbaya na wamelazwa katika hospitali ya Mkomaindo ni pamoja na
baba wa familia hiyo Jofrey Evance (43),mke wake Hadija Salumu (30),dada yake
Fidea Evance(40) pamoja na watoto wake wawili Husna Zuberi (8) na Godfrey Jofrey(10).
Alisema
kwa mujibu wa maelezo aliyoyatoa mganga Emele ni kwamba alitoa dawa hiyo kwa
wanafamilia hao ili waitumie kwa kuoga na kupaka kwenye miili yao na si
vinginevyo na baada ya kuwapa aliingia ndani ya nyumba yake lakini wanafamilia
hao walidanganywa na jirani yao aliyefahamika kwa jina la Mama Jane kuwa ili
kinga hiyo iwe ya kudumu na muda mrefu ni lazima waoge na wanywe maji yake.
Kwa
upande wao wauguzi wa zamu wa hospitali ya Mkomaindo waliowapokea wanafamilia
hao Prisca Mirumba wa wodi namba moja “B” ya wanaume na Sophia Erasto wa wodi
namba sita ya wanawake walisema kuwa waliwapokea wagonjwa hao jana usiku majira
ya saa 2:30 wakiwa wamepoteza fahamu huku baadhi yao wakitokwa na mapovu
kinywani.
Walisema
baada ya vipimo walibaini kuwa watu hao walipewa kimiminika kinachosadikika
kuwa ni sumu na waliwapa matibabu ya awali ingawa hadi sasa kwa mujibu wa
wauguzi hao ni kuwa hali za wanafamilia hao si ya kuridhisha.
Akizungumza
kwa tabu akiwa amelazwa kwenye wodi namba sita hospitali ya Mkomaindo mjini
Masasi Baba wa familia hiyo Jofrey Evance alisema kuwa chanzo cha yeye na
familia yake kwenda kwa mganga huyo kupata tiba ni baada ya watoto wake
kukumbwa na ugonjwa wa degedege.
Alisema
baada ya kufika kwa mganga huyo walipewa dawa hiyo ya Nyungu na kisha
kushwishiwa na jirani yao mama Jane wainywe dawa hiyo na kwamba mara baada ya
kunywa yeye pamoja na familia yake walipoteza fahamu na walijikuta wakiwa
hospitali ya Mkomaindo mjini Masasi.
Mwisho.
Hadija Salumu (30) ambaye ni mke wa Jofrey Evance akiwa amelazwa kwenye wodi namba sita katika hospitali ya Mkomaindo Masasi baada ya kunywa dawa inayosadikika kuwa ni sumu waliyopewa kutoka kwa mganga Emele mwenye umri wa miaka 17.
Mtoto HUSNA ZUBERI (8) ni miongoni mwa wanafamilia waliolazwa katika hospitali ya mkomaindo Masasi baada ya kunywa dawa yenye sumu waliyopewa na mganga wa tiba za asili.
Godfrey Jofrey (10) ni mtoto wa Bwana Jofrey Evance akiwa amelazwa wodi namba moja 'B"akiwa hajitambui kabisa baada ya kunywa dawa yenye sumu
Bi.Fidea Evance (40) dada wa Bwana Jofrey Evance naye ni miongoni mwa wanafamilia hao waliokunywa dawa kutoka kwa mganga wa tiba za asili yenye sumu akiwa katika wodi namba sita hospitali ya mkomaindo alikolazwa
BWANA JOFREY EVANCE BABA WA FAMILIA AKIWA AMEKAA KITANDANI WODINI
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD