TANGAZO
Na Clarence Chilumba,Masasi.
Watumishi wa serikali wilayani Masasi mkoani Mtwara wanaovaa
nguo fupi maarufu vimini yanayokwenda kinyume na maadili ya kitanzania
wameonywa kuacha mara moja tabia hiyo ambayo licha ya kudhalilisha kazi zao pia
ni aibu kwa mtumishi wa umma kuvaa mavazi kama hayo.
Pia jeshi la polisi
wilaya ya Masasi limeagizwa kufanya
operesheni maalumu katika kuwasaka na kuwafikisha mahakamani wale wote wanaotembea uchi kwa kuvaa nguo
fupi kwani kuvaa nguo fupi ni kosa la jinai ambalo muhusika anapaswa
kuchukuliwa hatua kali za kisheria.
Mkuu wa mkoa wa Mtwara Halima Dendego alitoa maagizo hayo
wakati anaongea na watumishi wote wa wilaya ya Masasi, Madiwani pamoja na viongozi
wa kimila wa kabila la wamakua (Mamwenye) ambapo amesema tabia za baadhi ya
vijana za kuvaa nguo fupi hazikubaliki kwenye jamii ya kitanzania.
Alisema ni aibu na fedheha kwa kijana ambaye ni mtumishi wa
umma kutofuata maadili ya utumishi wa umma ambao wengi wao huvaa nguo fupi
wanapokuwa makazini ambapo amewaagiza maofisa rasilimali watu kushughulika na
watu hao.
Dendego alielezea kusikitishwa kwake na vijana wa kiume
ambao wengi wao kwa sasa wamekuwa wakivaa nguo zinazoonesha sehemu ya nguo zao
za ndani kwa kushusha chini suruali zao (Mlegezo) kitu ambacho hakikubaliki
kuachwa kikiendelea kwa vijana nchini.
Alisema vijana wengi wamekuwa wakiiga kila kitu kinachofanywa
na nchi za mataifa ya magharibi ambapo amewaambia si kila kinachofanywa na
vijana hao ni cha maana kuigwa na badala yake waige masuala muhimu na ya msingi
katika maendeleo yao.
“Nyinyi vijana
mliopo hapa ndani naomba mnifikishie
ujumbe wangu kwa wenzenu kuwa
kutoka leo yeyote atakayevaa nguo fupi kwa wasichana na mlegezo kwa wavulana
atakamatwa na jeshi la polisi na hatimaye kufikishwa mahakamani na sheria
itachukua mkondo wake”.alisema Dendego.
Kwa mujibu wa Dendego alisema vijana wavae mavazi ya heshima
wakiwa kazini ama wanapokuwa kwenye shughuli zao binafsi na kwamba kwa kuvaa
kwao mavazi yanayokwenda kinyume na maadili ya kitanzania ni kujishushia heshima
na hadhi yao kwa wazazi wao na jamii kwa ujumla.
Aidha amewaomba watumishi walio kazini kwa muda mrefu watoe
maelekezo kwa vijana hao waachane na tabia zinazokwenda kinyume na maadili ya
utumishi wa umma ambao wengi wao wamekuwa wakivaa nguo fupi na zile zinazobana
mazingira ambayo husababisha kuonekana kwa maumbile ya miili yao.
Mwisho.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD