TANGAZO
MWENYEKITI WA MKUTANO WA WADAU WA ZAO LA KOROSHO NCHINI HEMEDI MKALI AKIZUNGUMZA WAKATI WA MKUTANO WA WATENDAJI NA VIONGOZI WA SEKTA YA KOROSHO MKOA WA MTWARA FEBRUARI 11,2015 KWENYE UKUMBI WA EMIRATES MJINI MASASI.
Na Clarence Chilumba,Masasi.
Zao la korosho ni miongozi
mwa mazao makuu ya biashara ambayo huliingizia Taifa fedha nyingi za kigeni
ambalo kwa siku za hivi karibuni limeingia kwenye kipindi ambacho wadau wengi
wa zao hilo wamekuwa wakilalamikia kushuka kwa thamani ya zao hilo.
Pamoja na jitihada kubwa zenye lengo la kumkomboa
mkulima wa zao la korosho zinazofanywa na serikali kwa kushirikiana na bodi ya
korosho nchini pamoja na wadau mbalimbali wa zao hilo bado wakulima wa zao hilo
wameendelea kubaki maskini wasijue cha kufanya.
Miongoni mwa
changamoto zinazotajwa na wadau wa sekta hiyo kuwa ni kikwazo kwa maendeleo kwa
wakulima ni pamoja na upinzani wa baadhi ya wadau katika kutekeleza mfumo wa
stakabadhi ghalani ambapo kumekuwepo na upotoshaji wa makusudi unaofanywa na
baadhi ya wafanyabiashara kwa ushirikiano na watendaji wa serikali wasiokuwa
waaminifu kueneza hofu kwa wakulima kuwa mfumo huo ni wa kinyonyaji.
Pia kutokana na
kusambazwa kwa propaganda hizo kuhusu mfumo wa stakabadhi ghalani zinazoenezwa
na wanunuzi na walanguzi wa zao hilo kumepelekea baadhi ya maeneo nchini
kushindwa kutekeleza ambapo matokeo yake ni kwa wakulima wa mkoa wa Pwani na
wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma kuuza zao la korosho kwa bei ndogo kuliko mikoa
na wilaya zinazotekeleza mfumo huo.
Uchunguzi uliofanywa
na gazeti hili umebaini kuwa kasi ndogo ya ubanguaji katika viwanda vilivyobinafsishwa
imepelekea korosho ya Tanzania kuuzwa zikiwa ghafi nje ya nchi na kwamba kutobanguliwa kwa korosho hizo nchini
kunawanyima fursa za ajira watanzania pamoja na kushusha thamani ya zao hilo.
Ubinafsishwaji wa
viwanda hivyo ulitokana na mabadiliko ya kisera na kiuchumi yaliyopelekea
viwanda hivyo kubinafsishwa huku waliovinunua wakitakiwa kuendeleza shughuli za
ubanguaji wa zao hilo lakini katika hali
ya kushangaza viwanda hivyo vimeshindwa kutimiza malengo yaliyokusudiwa huku
baadhi ya majengo ya viwanda hivyo yakitumika kama maghala ya kuhifadhia bidhaa
za madukani za wafanyabiashara hao.
Aidha ushindani mdogo
wa bei unaotokana na uchache wa masoko ya zao hilo ni sababu nyingine kubwa
inayoendelea kudidimiza ndoto za wakulima wa zao hilo nchini ambao ni kwa muda
mrefu sasa wamekuwa wakipaza sauti zao kwa vyombo vyenye mamlaka ingawa hadi
sasa hakuna mabadiliko yoyote katika tasnia hiyo muhimu kwa maendeleo ya nchi.
Bei ya zao la korosho
ghafi imekuwa ikipanda na kushuka kulingana na ufinyu wa masoko yanayonunua zao hilo duniani kunakopelekea
hasara kubwa kwa wakulima wa zao la korosho nchini licha ya kuwepo kwa gharama
kubwa za utayarishaji wa zao hilo kutokaka na kupanda kwa gharama za
pembejeo ambazo baadhi ya hizo zimekuwa
zikipigwa vita na wakulima hao kwa madai kuwa hazifai.
Kwa mujibu wa taarifa
iliyotolewa na mwenyekiti wa mkutano wa wadau wa bodi ya korosho nchini Hemedi
Mkali wakati wa mkutano wa watendaji na viongozi wa sekta ya korosho mkoa wa
Mtwara februari 11 mjini Masasi ilisema kuwa kuwepo kwa mabadiliko ya majina ya
viuatilifu kunakotokana na mabadiliko ya majina ya makampuni yanayoshinda
zabuni za usambazaji wa pembejeo za ruzuku ni changamoto nyingine ya zao hilo nchini.
Taarifa hiyo
iliendelea kudai kuwa kutokana na mfumo wa ununuzi wa pembejeo hizo iko dhana
mbaya kutoka kwa wakulima kuwa bodi ya korosho nchini huagiza pembejeo kutoka
kwa makampuni hayo ambazo wakulima hawazihitaji ambapo ukweli ni kwamba bodi
pamoja na mfuko wa kuendeleza zao la korosho (WAKFU) huratibu mahitaji ya
wakulima kwa kushirikiana na Halmashauri za wilaya kwa kuzingatia viuadudu au
viasili vya viuatilifu vinavyohitajika ambapo hutangazwa kupitia utaratibu wa
zabuni.
Taarifa ilisema kuwa
msambazaji mwenye viuatilifu vyenye ubora uliothibitishwa na mamlaka husika
anaruhusiwa kushiriki katika zabuni na yeyote atakayeshinda kwenye zabuni hiyo
hupewa fursa ya kusambaza madawa hayo kwa wakulima huku wakulima hao wakiaswa
kutosikiliza propaganda zinazosambazwa na walanguzi wa zao hilo wasiowatakiwa
mema wakulima.
Katika kuhakikisha
kila mkulima anapata pembejeo za kilimo cha zao hilo kwa wakati ilikubaliwa
kuwa kamati za pembejeo za wilaya zinazozalisha zao la korosho ziwe makini
katika uteuzi wa mawakala ili kupata wenye sifa kama inayoelekezwa kwenye
muongozo wa usambazaji wa pembejeo na kwamba ni vyema mawakala wakapatikana kwa
kutoa matangazo ya wazi kwa waombaji.
Pamoja na kuwepo kwa
changamoto hizo ambazo ni dhahiri kuwa zinamkandamiza mkulima serikali kwa
kushirikiana na mfuko wa WAKFU pamoja na wadau wa zao hilo wameweka mikakati
kadhaa yenye lengo la kumkomboa mkulima kutoka kuwa maskini na kufikia kwenye
hatua ambayo ataweza kufurahia matunda ya kilimo cha zao hilo.
Miongoni mwa mikakati
hiyo ni pamoja na kuongeza uzalishaji kutoka wastani wa tani 120,000 za sasa
hadi kufika tani 300,000 kufikia mwaka 2016 kwa kuhamasisha maeneo yote
yanayolima zao hilo nchini kuongeza uzalishaji sambamba na kupanda miche bora
ya korosho yenye sifa za kuzaa kwa wingi na yenye uwezo wa kuvumilia magonjwa
na hali ya hewa.
Pia bodi ya korosho
Tanzania imenzisha kampeni ya kuhamasisha wakulima kukusanya korosho kwenye maghala
bila kutegemea mikopo kutoka kwenye taasisi za fedha ili kupunguza utegemezi na
kwamba katika msimu wa mwaka 2013/2014 vyama zaidi ya 13 mkoani Mtwara vimeuza
korosho zake bila kukopa fedha benki.
Aidha serikali kwa
kushirikiana na bodi ya korosho nchini iko mbioni kujenga viwanda vitatu vya kubangua korosho vitakavyomilikiwa na
wadau wa korosho kwa utaratibu maalumu wa kibiashara ambapo kwa kuanzia viwanda
hivyo vitajengwa katika miji ya
Mtwara,Mkuranga na Tunduru ili kuongeza kasi ya ubanguaji wa zao hilo nchini.
Tasnia ya zao la
korosho nchini inayo fursa ya kubwa ya kukuza zao hilo kwa kuongeza uzalishaji
wenye lengo la kuongeza mchango wa pato la Taifa huku serikali,wadau pamoja na
mfuko wa kuendeleza zao hilo wakiaswa kuacha mivutano na migongano isiyo na
maana ili maendeleo ya zao hilo yaweze kufikiwa.
Mwisho.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD