TANGAZO
Na Clarence
Chilumba,Masasi.
Mkuu wa mkoa wa Mtwara
Halima Othmani Dendego ameapa kula sahani moja ikibidi kuwashikia bakora baadhi
ya watendaji wake mkoani humo watakaobainika
kutafuna fedha za wakulima wa zao la korosho zinazotolewa
na mfuko wa kuendeleza zao hilo nchini
WAKFU.
Pia amekiri kuwepo kwa
siasa nyingi kwenye zao la korosho ambapo imefikia hatua kwa baadhi ya viongozi
wanaoonekana kusimamia haki za wakulima wa zao hilo kupewa vitisho vya
kukatisha uhai wao kwa kile kinachodaiwa kuingilia maslahi ya baadhi ya
wafanyabiashara wanaowadhulumu wakulima wa zao la korosho.
Aidha ameelezea msimamo
wake wa dhati kuwa yuko tayari kwa lolote litakalojitokeza mbele yake katika harakati
hizo zenye lengo la kuwakomboa wakulima wa zao hilo ambao kwa miaka mingi wamekuwa
wakidhulumiwa mazingira ambayo husababisha kubaki wakiwa maskini wa kutupwa.
Aliyasema hayo juzi wakati
anafungua mkutano wa watendaji na viongozi wa sekta ya korosho mkoa wa Mtwara
uliofanyika kwenye ukumbi wa Emirates mjini Masasi mkutano uliowahusisha
viongozi wa bodi ya korosho nchini, wakuu wa wilaya za mkoa wa Mtwara pamoja na
wakulima na wadau wa zao hilo mkoani Mtwara.
Alisema mikoa ya kusini ni
miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa zao la korosho nchini lakini cha kushangaza
wakulima wa mikoa hiyo wameendelea kubaki wakiwa maskini wa kipato huku
wafanyabiashara na baadhi ya watendaji wa serikali na wa bodi ya korosho
wakineemeka na faida ya zao hilo.
“Nawaagiza watendaji wangu
kuachana na tabia za wizi kwenye fedha
zinazotolewa na mfuko wa WAKFU kwa wilaya zote mkoani Mtwara…kwa hili naapa nitasimama
bila woga,siogopi vitisho na kwamba niko tayari kupambana na wezi wote katika
mkoa wangu wanaowaibia wakulima wa zao la korosho”.Alisema Dendego kwa uchungu.
Alisema fedha zinazoletwa
na mfuko wa kuendeleza zao la korosho nchini zitumike kama zilivyokusudiwa ambapo
amewaagiza wakuu wa wilaya mkoani humo kusimamia fedha hizo ili wakulima waweze
kunufaika na matunda ya nguvu zao.
“Hii ni fedheha hizi fedha
haziletwi ili zichezewe…kwani hata hizo Halmashauri mnazoziona zikitekeleza
miradi ya maendeleo zinategemea ushuru kutoka kwenye zao la korosho na kwamba
kikao hiki cha leo iwe mwisho wa wizi huu ambao ni dhahiri unamfanya mkulima
kuendelea kubaki mnyonge”.Alisema Dendego.
Kwa mujibu wa mkuu huyo wa
mkoa alisema ofisi ya mkoa wa Mtwara iko tayari kushirikiana na makundi yote
yanayohusika katika uendelezaji wa zao la korosho katika kutafuta fursa za
masoko popote duniani ili kuifanya korosho ya Tanzania iwe kwenye viwango vya
kimataifa.
Alisema wakulima wa zao
hilo wamekuwa wakitumia fedha nyingi wakati wa uandaaji wa zao hilo na kwamba
ni vyema serikali na wadau wakaunga mkono jitihada hizo zinazofanywa na
wakulima hao ili kuwakomboa kiuchumi.
Mwisho.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD