TANGAZO
Na Clarence Chilumba,Nanyumbu.
SERIKALI kupitia TAMISEMI imetoa vitabu vya masomo ya sayansi
vipatavyo 6477 kwa Halmashauri ya wilaya ya Nanyumbu mkoani Mtwara lengo likiwa
ni kukabiliana na tatizo la upungufu wa vitabu vya masomo hayo katika shule za
sekondari nchini.
Akizungumza na wandishi wa habari hivi karibuni ofisini kwake
kaimu Ofisa elimu sekondari wa wilaya hiyo, Jouiser Jellah alisema
kuwa vitabu hivyo ni sehemu ya juhudi na mkakati wa Raisi Jakaya Kikwete katika
kukabiliana na tatizo la vitabu vya masomo ya sayansi nchini.
Alisema vitabu hivyo vitasambazwa katika shule zote za sekondari
zilizopo katika wilaya hiyo ambazo ni 12 na kwamba tatizo la upungufu wa vitabu
kwenye shule hizo litakuwa limemalizika hivyo itasaidia kutoa fursa kwa
wanafunzi kuweza kufanya vizuri kwenye masomo hayo.
“Changamoto kubwa kwetu ni ruzuku hadi sasa serikali imekuwa
ikitoa ruzuku ndogo ambayo haiendani na mtiririko chanya wa ruzuku inavyopaswa
kutolewa hivyo tatizo hili linakwamisha mipango yetu mingi katika kuinua
kiwango cha elimu wilayani hapa,”alisema Jellah.
Aliongeza kuwa awali shule hizo zilikuwa na changamoto ya upungufu
wa vitabu mbalimbali ikiwemo vya masomo ya sayansi lakini kupitia vitabu hivyo
kwa upande wa masomo ya sayansi kwa sasa tatizo litakuwa limemalizika ambapo
ameipongeza serikali kwa kutoa vitabu hivyo.
Aidha alisema idara ya elimu sekondari kwa sasa ina upungufu wa
walimu wa masomo ya sayansi wapatao 48 hali inayochangia wanafunzi wanaosoma
masomo hayo kukosa walimu wa kutosha wa kuwafundisha masomo hayo.
Kwa upande wa changamoto ambazo zinakwamisha kuinua kiwango cha
elimu katika wilaya hiyo Jellah alisema kuwa ni mwamko mdogo wa jamii kushindwa
kuwasomesha watoto wao kwa sababu ambazo si za msingi.
Alisema changamoto nyingine katika idara ya elimu sekondari
katika wilaya hiyo ni pamoja na ukosefu wa thamani za ofisi ambapo katika
baadhi ya shule zinakabiliana na tatizo hilo hali ambayo inashusha morari kwa
walimu kufundisha kwa ufanisi zaidi.
Jellah alisema kuhusu mikakati iliyowekwa katika idara hiyo ni
kuhakikisha idara inashirikiana na wadau mbalimbali katika kusaidia kuendesha
shule ili kwa pamoja kuweka mikakati iliyo bora na kutatua changamoto zilizopo
hatimaye kuinua kiwango cha taalumu wilayani humo.
Kwa upande wake mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri hiyo,Ally
Kassinge alisema kuwa Halmashauri yake itahakikisha kuwa inakuwa na mikakati
iliyobora kwa ajili ya kuinua kiwango cha elimu kama inavyotakiwa kwa kuwa watendaji
wa Halmashauri wamekuwa shupavu katika utendaji kazi wao.
Mwisho
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD