TANGAZO
MWALIMU MKUU MATATANI UJENZI WA MAABARA
Mwenyekiti
wa Halmashauri ya mji wa Masasi mkoani Mtwara Andrew Mtumusha amemuagiza
mkurugenzi wa Halmashauri hiyo kumchukulia hatua za kinidhamu mkuu wa shule ya
sekondari ya kutwa ya Mwenge Mtapika Aziz Mwakalasi kwa kutosimamia vizuri ujenzi
wa maabara shuleni hapo.
Aidha
ameagiza kifanyike kikao cha dharula
(leo) kitakachomuhusisha mwenyekiti wa bodi wa shule hiyo,mratibu elimu kata wa
kata hiyo,ofisa mtendaji wa kata pamoja na mwalimu mkuu huyo ili kubaini sababu
za kusuasua ujenzi wa maabara katika shule hiyo.
Pia
mwenyekiti huyo alikasirishwa na kitendo cha mwalimu huyo kuondoka shuleni hapo
kuelekea mkoani Mtwara bila kuaga kwa uongozi wa Halmashauri na kwamba kitendo
hicho ni utovu wa nidhamu.
Mtumusha
alitoa agizo hilo mwishoni mwa wiki mara baada ya kufanya ziara ya kushtukiza shuleni
hapo iliyokuwa na lengo la kukagua ujenzi wa maabara ambapo alijionea mwenyewe
uzembe wa usimamizi unaofanywa na mkuu huyo wa shule.
Alisema
miradi mingi katika shule hiyo ikiwemo ujenzi wa nyumba ya mwalimu ambayo hadi
sasa haijakamilika utekelezaji wake umekuwa wa kusuasua mno licha ya
Halmashauri kutoa fedha za ujenzi wa miradi hiyo.
Alisema
kuwa mwalimu huyo ameshindwa kuendana na kasi ya ujenzi wa maabara hivyo ni
dhahiri kwamba hapaswi kuachwa hivi hivi bila kuchukuliwa hatua za kinidhmu ili
iwe fundisho kwa wakuu wengine wa shule ambao ni wazembe.
“Kiukweli
nimekasirishwa sana na uzembe alioufanya huyu mwalimu, hivyo nakuagiza mkurugenzi
haraka iwezekanavyo mwalimu huyu aitwe ofisini kwako ili aje atoe majibu ni kwa
nini ujenzi wa maabara hii bado uko kwenye hatua ya msingi wakati fedha tayari ameshapatiwa”Alisema.
Mtumusha
alisisitiza kuwa mkurugenzi pamoja na watendaji wake waache tabia ya kuoneana
aya na kufanya kazi kirafiki katika kutekeleza majukumu ya kila siku hasa kwa
wakati huu ambapo Halmashauri zote nchini ziko kwenye hekaheka ya kutekeleza
agizo la Raisi Kikwete.
Kwa
mujibu wa Mtumusha alisema vitendo vya uzembe kwa watendaji ndani ya
Halmashauri hiyo havina nafasi na kwamba ni vyema sasa wakafanya kazi kwa
ushirikiano ili kuondoa migongano ambayo inaweza kujitokeza pale tu
wataposhindwa kutimiza majukumu yao.
Mwisho.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya mji wa Masasi mkoani Mtwara Andrew Mtumusha (Mwenye kofia) akitoa maelekezo mbela ya mafundi wanaojenga maabara kwenye shule za sekondari za halmashauri hiyo wakati wa ziara yake aliyoifanya mwishoni mwa wiki.
Ujenzi wa jengo la maabara linalosuasua lililomtia matatani mwalimu mkuu.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD