TANGAZO
DC
AAPA KULA SAHANI MOJA NA WAZAZI PAMOJA NA VIONGOZI WAZEMBE
Mkuu wa wilaya ya masasi
mkoani Mtwara Farida Mgomi ametoa onyo
kali kwa wazazi wa watoto waliochaguliwa
kujiunga na kidato cha kwanza kwa mwaka wa masomo wa 2014/2015 kuwa hatosita
kuwachukulia hatua kali za kisheria ikiwa ni pamoja na kuwafikisha mahakamani
wazazi hao watakaothubutu kuacha kuwapeleka watoto wao shuleni.
Pia
ametoa agizo kwa watendaji wa kata na vijiji wilayani humo
kufuatilia chanzo cha wanafunzi wengi kutoripoti shuleni bila sababu za msingi
huku akiwapa rai kuwa endapo baadhi yao
watabainika kuwa ni sababu ya utoro huo kwenye maeneo yao basi wajiandae
kutafuta kazi zingine zitakazowafaa kabla hajawachukulia hatua kali.
Aidha
alisema inashangaza na inatia aibu kwa wilaya ya Masasi ambayo imetoa viongozi wengi
wa kitaifa huku ikiwa haina tatizo la vyumba vya madarasa kuona kuwa idadi
kubwa ya wananfunzi wanaochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza kila mwaka
huwa hawaripoti shuleni kutokana na uzembe wa baadhi ya wazazi.
Aliyasema
hayo jana wakati wa mahojiano maalumu na gazeti hili lililotaka kufahamu wilaya
ya Masasi imejipangaje katika kukabiliana na idadi kubwa ya wanafunzi ambao
kila mwaka huchaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza lakini cha kushangaza
wengi wao hawaripoti kwa kisingizio kutoka kwa wazazi wao cha hali ngumu ya
maisha.
Alisema wazazi waache kutoa
visingizio visivyo na mantiki yoyote vya kukosa uwezo wa kuwapelekea watoto wao
shuleni huku wakitumia pesa nyingi wakati watoto hao wanapomaliza shule ya
msingi kwa kuandaa chakula, mavazi ya gharama pamoja na pombe wakifurahia
watoto wao kumaliza elimu ya msingi.
“Ni jambo la kushangaza
na linalosikitisha kwa baadhi ya wazazi wilayani Masasi ambao wamekuwa na tabia
ya kutumia fedha nyingi wakati ule watoto wao wanapomaliza elimu ya
msingi…lakini kipindi cha watoto hao kuwapeleka sekondari wazazi hao hushindwa
kumudu gharama hizo kwa kisingizio cha hali ngumu ya maisha na kwamba kwa hili
halipaswi kuvumiliwa ni lazima mwaka huu tulikomeshe”.Alisema.
Mgomi alisisitiza kuwa
wilaya ya Masasi haina tatizo la vyumba vya madarasa na kwamba wanafunzi wote
wapatao 3897 waliochaguliwa kujiunga na kidato kwa kwanza mwaka huu wote watapata
nafasi ya kusoma.
Alisema
hatomuonea haya mzazi yeyote ama kiongozi yeyote yule ambaye kwa namna moja ama
nyingine atachangia kuzorotesha jitihada za wilaya ya Masasi za kuhakikisha
kuwa watoto wote wanaripoti shuleni ifikapo januari 31, 2015 na kwamba ameapa
kula nao sahani moja ili iwe fundisho kwa wengine.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wenyeviti wa
Halmashauri zinazounda wilaya ya Masasi Andrew Mtumusha ambaye ni mwenyekiti wa
Halmashauri ya mji wa Masasi pamoja na Juma Satma wa Halmashauri ya wilaya ya Masasi
walikiri kuwa tatizo hilo Masasi ni kubwa na kwamba hawaelewi ni kwa nini
wazazi wengi wilayani humo hawatambui umuhimu wa elimu wakati wamekuwa
wakitumia fedha nyingi kwenye sherehe kama vile jando na unyago pamoja na
harusi.
Walisema
bado msimamo wao ni kuwataka wazazi ambao watoto wao wamechaguliwa kujiunga na
kidato cha kwanza mwaka huu wawapeleke shuleni na kwamba mzazi ambaye atakiuka
amri hiyo ambayo ni ya kisheria basi hatua kali zitachukuliwa dhidi yake.
Walisisitiza
kuwa wakati umefika kwa madiwani wa halmashauri hizo mbili kutambua kuwa hilo ni jukumu lao na kwamba
wanapaswa kutoa msukumo mkubwa ikibidi
kutumia nguvu kwenye maeneo yao katika kupambana na baadhi ya wazazi ambao wamekuwa ni kikwazo ili kukinusuru kizazi hiki kinachoelekea kupotea
kwa kukosa elimu.
“Sisi
Kama wenyeviti wa Halmashauri hizo tayari tumejiwekea mikakati madhubuti ikiwa
ni pamoja na kuunda kikosi kazi kitakachofanya operesheni maalumu ya nyumba kwa
nyumba ili kuwasaka wale wote watakaosababisha wanafunzi hao kutoripoti shuleni
kwa wakati”.Walisema.
Wakitoa
maoni yao baadhi ya wananchi waliozungumza na gazeti hili wilayani Masasi kuhusu sababu ambazo husababisha wanafunzi
wengi kutoripoti shuleni wengi wao waliinyooshea kidole idara ya mahakama kwa
kile walichodai kuwa imekuwa
ikidhoofisha jitihada zinazofanywa na watendaji wa serikali za vijiji na kata kwa kutowachukulia hatua kali za kisheria wazazi ama walezi wanaosababisha watoto wao
kutoripoti shuleni.
Waliendelea
kusema idara ya mahakama imekuwa ikifanya kazi zake kwa dharau kubwa kwa
watendaji hao wa ngazi ya vijiji na kata kwa kuwaachia huru watuhumiwa ambao
wamethibitika kusababisha wanafunzi kutoripoti shuleni bila maelezo na kwamba
wakati mwingine hutoa majibu yanayokatisha tamaa kuwa hakuna kifungu chochote
cha sheria kilichoainisha kwamba anayesababisha mwanafunzi asiende shuleni apewe
adhabu.
Walisema
mbaya zaidi hata wale wanaowapa ujauzito watoto hao wamekuwa wakiachwa huru
licha ya watendaji hao kuwafikisha watuhumiwa kwenye vyombo vya maamuzi
mazingira huku baadhi ya wazazi nao wakiingia lawamani kwa kuchukua fedha
kidogo kutoka kwa watuhumiwa.
Takwimu
zinaonesha kuwa kila mwaka wilaya ya Masasi mkoani Mtwara yenye jumla ya shule
35 za sekondari imekuwa ikifaulisha kwa kiwango cha juu huku wanafunzi wengi
wakichaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza lakini changamoto kubwa inayopaswa
kutafutiwa ufumbuzi ni ya wanafunzi hao kutoripoti shuleni huku kundi kubwa la
watoto hao hasa wa kike likielekea Dar es salaam kwa ajili ya kufanya kazi za
ndani.
Mwisho.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD