TANGAZO
AUAWA
KWA KUPIGWA MAWE NA HATIMAYE KUCHOMWA MOTO
Na Clarence Chilumba, Ruangwa
Mkazi wa kitongoji cha Mnele kijiji cha Chinongwe B katika
kata ya Chinongwe wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi Longino John (35) ameuawa na
wananchi wenye hasira kali kwa kupigwa mawe na hatimaye kuchomwa moto kwa madai
ya kumpiga na kumjeruhi Mendrati Chinguile (63) ambaye ni mlemavu wa macho.
Tukio hilo la kusikitisha limetokea jana majira ya saa 7:00
mchana huko kwenye kitongoji cha Mnele kilichoko katikati ya kijiji cha
Chinongwe na Luchelegwa wilayani Ruangwa ambapo kundi kubwa la watu wenye
hasira walimpiga mawe kijana huyo na hatimaye kumchoma moto kwa kutumia mafuta
ya petroli.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo kamanda wa polisi mkoa
wa Lindi Renatha Mzinga alisema jana majira ya saa 7:00 mchana kijana huyo
aliuawa na wananchi hao wa kitongoji cha Mnele kwa madai ya kuchoshwa na tabia
yake ya ubabe aliyokuwa nayo marehemu hasa pale alipokuwa amelewa.
Alisema kabla ya kifo chake marehemu alikuwa ni mtu wa
matukio ya ajabu kijijini hapo ikiwemo ulevi wa kupindukia, wizi pamoja na
matukio yake ya kupiga watu bila sababu za msingi na kwamba juzi (Alhamisi)
alimpiga kwa mapanga na kumjeruhi kichwani mtoto wa mzee Mendrati Chinguile
aitwaye Amosi Cleophas (25) na kukimbizwa katika hospitali ya misheni ya Ndanda
na hatimaye aliruhusiwa na hali yake inaendelea vizuri.
Mzinga alisema jana asubuhi majira ya saa 2:00 akiwa amelewa
marehemu alienda nyumbani kwa mzee Mendrati Chinguile ambaye ni mlemavu wa
macho tangu miaka ya 1990 na kwamba alipofika alianza kudai kuwa amekuja
kufuata vyombo vyake vya ndani ambavyo kwa mujibu wa mashuhuda walidai kuwa ni
taarifa za uzushi na kwamba hakuwa anamdai chochote mzee huyo bali ni hasira
ambazo alikuwa nazo dhidi ya mtoto wa mzee huyo.
Alisema malumbano hayo baina yake na mzee huyo yaliendelea
bila mafanikio yoyote na hatimaye aliamua kuingia ndani na kumtoa nje ya nyumba
yake mzee Mendrati na kuanza kumpiga kichwani kwa kutumia kipande kikubwa cha
mti alichokuja nacho mazingira yaliyomsababishia mzee huyo majeraha makubwa
kichwani na alikimbizwa na wasamaria wema katika hospitali ya Ndanda na kupata
matibabu huku hali yake ikiwa bado inaendelea kuimarika.
Kwa mujibu wa kamanda
mzinga alisema wasamaria wema ndio waliomuokoa mzee huyo asiuawe na kijana huyo
kwa kuwa nyumba yake iko nje kidogo na kijiji na kwamba mara baada ya kumkamata
walianza kumpiga kwa mawe na hatimaye walifanikiwa kumuua na ndipo waliamua
kuchukua mafuta ya petrol kutoka kwa waendesha bodaboda na hatimaye
walifanikiwa kumchoma kwa moto.
Alisema polisi walifika eneo la tukio majira ya saa 11:jioni
na baada ya kufanya mahojiano na baadhi ya
watu kijijini hapo waliamuru mwili wa marehemu Longino John uzikwe na
majira ya saa 12:30 jioni marehemu alizikwa na watu wachache waliofika kwenye
eneo hilo na kwamba hadi sasa hakuna mtu yeyote anayeshikiliwa na jeshi la
polisi huku upelelezi ukiendelea wa kuwabaini waliofanya tukio hilo la kinyama.
Mwisho.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD