Loading...
ADVERTISE WITH US ON THIS BLOG.CALL +255 714 789 592/ +255 682 997 767/ +255 752 944 022

Je,Wewe Ni Mkazi Wa Masasi? Ona Aibu Mtoto Wako Kukaa Chini,Jitolee Kutengeneza Dawati,Masasi Ni Mimi Na wewe.

TANGAZO
MKURUGENZI wa Halmashauri ya Mji wa Masasi,Fortunatus Mathew Kagoro (Picha ya Maktaba).

TAARIFA FUPI KUHUSU HALI YA MADAWATI HALMASHAURI YA MJI WA MASASI.
Katika kutekeleza agizo la  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.John Pombe Magufuli alilolitoa Machi 16,2016 wakati anawaapisha wakuu wa mikoa  kuhusu utekelezaji wa elimu bila malipo,Rais aliwataka  wakuu hao wa mikoa kuhakikisha wanasimamia upatikanaji wa madawati ifikapo Juni mwaka huu.

Mkoa wa Mtwara chini ya uongozi wa mkuu wa mkoa huo Mheshimiwa Halima Dendego umedhamiria kukamilisha suala la madawati ifikapo Mei 2016 kwa Halmashauri zote tisa zinazounda mkoa huo Masasi mji ikiwemo kutumia njia mbalimbali ili wanafunzi wote wakae kwenye madawati.

Katika kikao kilichoitishwa Februari, mwaka huu na mkuu wa mkoa wa Mtwara baada ya kubaini changamoto hizo,  wakurugenzi wa halmashauri na wakuu wa wilaya waliagizwa kuhakikisha wanashughulikia changamoto hizo hasa uhaba wa madawati ambapo kwa ujumla mkoa wa Mtwara una  upungufu wa madawati 35,406.

Kwa upande wa Halmashauri ya mji wa Masasi tayari mchakato wa upatikanaji wa madawati hayo umeanza kwa kutumia rasilimali zilizopo pamoja na mapato ya ndani sambamba na kushirikisha wadau mbalimbali wa maendeleo zikiwemo taasisi za serikali,taasisi binafsi za kifedha,wafanyabiashara pamoja na wananchi wote kwa ujumla kwa lengo la kuhakikisha kuwa ifikapo Mei 2016 watoto wote wanaokaa chini wawe wamepata madawati.

HALI HALISI:

Kutokana na kuwepo kwa mpango wa elimu bure bila malipo  wazazi wamekuwa wakijitokeza kwa wingi kupeleka watoto shule mazingira yaliyopelekea kuwepo kwa idadi kubwa ya wanafunzi kwenye shule za msingi na sekondari ambapo kwa upande wa shule za msingi jumla ya wanafunzi 20,957 waliandikishwa kuanza darasa la kwanza.

Aidha kutokana na idadi kubwa ya wanafunzi kuandikishwa kwenye shule zote 33 zilizopo katika Halmashauri hiyo kumekuwa na changamoto kubwa kwa baadhi ya shule hizo wanafunzi wake kukaa chini kutokana na uhaba wa madawati.

Halmashauri ya mji wa Masasi inahitaji jumla ya Madawati 6975,huku yaliyopo ni madawati 4646 na pungufu ni madawati 2329 hivyo ili wanafunzi wote waweze kukaa kwenye madawati Halmashauri inahitaji kiasi cha shilingi Milioni 349,350,000 ambapo hadi sasa kazi mbalimbali zimekuwa zikifanywa na Halmashauri katika kutatua changamoto hiyo ya madawati.


HATUA ZILIZOCHUKULIWA NA HALMASHAURI:

Halmashauri ya mji wa Masasi imefanya jitihada mbalimbali katika kukabiliana na changamoto hiyo ya upungufu wa madawati na miongoni mwa hatua  hizo ni pamoja na:
  • ·   Kuanzisha Kampeni inayoitwa “ONA AIBU MTOTO WAKO KUKAA CHINI SHULENI…JITOLEE KUTENGENEZA DAWATI…MASASI NI MIMI NA WEWE”.

  • ·       Upasuaji wa Mbao na Boriti kwa kutumia miti iliyopo eneo la Halmashauri ambapo hadi sasa jumla ya mbao 119 pamoja na Boriti 65 zimepatikana.

  • ·      Kuandika barua za maombi ya mchango kwa vyama vya ushirika vilivyopo Halmashauri ya mji wa Masasi.

  • · Maombi kwa taasisi za kifedha ikiwemo NMB ambao wameahidi kutengeneza madawati kwa awamu tano na kwa awamu ya kwanza watatengeneza madawati kwa shule moja ingawa hawakueleza idadi ya madawati wataakayotengeneza.

  • ·   Kuomba mchango kwa Wakala wa huduma za misitu kanda ya kusini (TFS) ambao wamekubali kutoa msaada wa madawati 40 ambayo tayari yameanza kutengenezwa.

  • · Mazungumzo kati ya Halmashauri na wafanyabiashara wa mazao mchanganyiko ambao wamekubali kuchangia kiasi cha shilingi 10 kwa kila kilo moja wakati wa ununuzi wa mazao hayo.

Kwa upande wa idara ya elimu sekondari pia kumekuwepo na changamoto kadhaa za elimu kwenye shule zake Tisa (9) zilizopo kwenye Halmashauri ya mji wa Masasi ambapo kwa sasa changamoto kubwa iliyopo ni upungufu wa viti na madawati.

Mahitaji ambayo kwa sasa yanahitajika ni pamoja na meza 3664,viti 3664 na kwamba meza zilizopo ni 3078 na viti 2657 huku upungufu ukiwa   ni meza 586 na viti 1007. Kushuka kwa upungufu huu ni kutokana na juhudi za Halmashauri za kukarabati viti na meza mbovu.

WITO:

Hivyo ukiwa kama mdau wa elimu tunaomba msaada wako wa hali na mali katika kuhakikisha kero hii ya madawati kwa watoto wetu ambao baadhi yao wamekuwa wakikaa chini kwa kukosa madawati inakwisha ili kutekeleza agizo la Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania Dk.John Pombe Magufuli.

Ujumbe: “ONA AIBU MTOTO WAKO KUKAA CHINI SHULENI…JITOLEE KUTENGENEZA DAWATI…MASASI NI MIMI NA WEWE”.

Clarence Chilumba,
Ofisa Habari Halmashauri ya Mji Masasi,
03/04/2016.




TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD
Newer Posts Older Posts
© Copyright Mtazamo Mpya | Designed By FAHARI YA TANZANIA
Back To Top