TANGAZO
Sheikh Alli Dino Tahir wa Kanda ya Kusini Jumuiya ya Ahmadiya. |
Na Clarence
Chilumba,Masasi.
Amir na mbashiri mkuu wa
jumuiya ya waislamu wa Ahmadiya nchini Tahir Chandry amewataka waumini wa
jumuiya hiyo kumtumikia mungu kikamilifu kwa kufuata misingi na kanuni
zilizowekwa katika Quran tukufu kwa lengo la kuleta amani na mshikamano
miongoni mwa waislamu wa jumuiya hiyo duniani.
Akizungumza jana mjini
Masasi wakati wa mkutano mkuu wa mwaka wa jumuiya hiyo kwenye viwanja vya
msikiti wa Ahmadiya mjini humo alisema lengo la kuanzishwa kwa jumuiya hiyo ni
kuwaunganisha waumini wote wenye kufuata amri zilizowekwa na mwenyezi mungu.
Alisema mafundisho kutoka
katika vitabu vitakatifu mungu amehimiza amani,upendo,na mshikamano kwa wale
wote wanaomwanini kwa nia thabiti na kwamba hali ilivyo kwa sasa ni tofauti
kwani kumezuka makundi mbalimbali ya dini ya kiislamu yapatayo 72 ulimwenguni
kote huku kila moja likijinadi kuwa ndilo linalofuata maagizo yaliyopo kwenye
kitabu kitakatifu cha Quran tukufu.
Alisema uelewa mdogo kuhusu
dini ya kiislamu kwa baadhi ya waumini wa dini hiyo ndiko kulikopelekea kuwepo
kwa tofauti kubwa kote duniani mazingira ambayo hupelekea waislamu kuuana
wenyewe kwa wenyewe ikiwemo mauaji yanayotekelezwa na makundi mbalimbali kama
vile Boko Haram,Al Shabab na mengineyo.
Kwa mujibu wa Amir na
mbashiri mkuu wa jumuiya ya Ahmadiya nchini Tahir alisema wakati umefika kwa
waislamu kufuata kamba iliyo ya kweli ya mwenyezi mungu na kwamba wao kama
jumuiya moja ya kazi kubwa wanayoifanya kwa sasa ni kuhubiri amani kote
ulimwenguni ili waislamu wamrudie mungu wao sambamba na kuacha mapigano ya kila
siku yanayosababisha maelfu ya waislamu kupoteza maisha.
“Kila siku kupitia vyombo
vya habari vya kimataifa tumekuwa tukishuhudia mauaji ya waislamu kule
Yemen,Pakistan…lakini ukiangalia kiundani zaidi wanaotekeleza mauaji yale ni
waislamu ambao huua waislamu wenzao na wakati mwingine hata wasio waislamu
huuawa kwa nini tuendelee kuuana huku kamba sahihi ya uzima ipo inayofuata
ukhalifa”.alisema Amir Chandry.
Akizungumzia namna jumuiya
yake inavyounga mkono jitihada za serikali ya Tanzania katika kuboresha miundo
mbinu mbalimbali ikiwemo elimu,afya na maji Amir Chandry alisema wamefanikiwa
kuchimba na kujenga visima vya maji katika baadhi ya maeneo nchini ikiwemo
mikoa ya Mtwara,Morogoro,Dodoma,Singida pamoja na Arusha.
Alisema mbali na kujenga
visima vya maji pia jumuiya ya waislamu wa Ahmadiya nchini imekuwa ikitoa
misaada katika shule mbalimbali za sekondari kama vile kompyuta,madawati pamoja
na vitabu kwa wanafunzi wa shule hizo na kwamba kote wanakopita hutoa mahubiri
kuhusu amani na namna ya kuifuata kamba bora ya imani kitu ambacho amekiri kuwa
ni tofauti na baadhi ya jumuiya zingine.
Kuhusu uchaguzi mkuu wa
Tanzania Oktoba mwaka huu Amir alisema wao kama jumuiya ya Ahmadiya wako tayari
kufuata kanuni na taratibu za nchi kwa Rais yeyote ambaye atachaguliwa na
watanzania na kwamba wao kama jumuiya ya kidini nchini hawawezi kuwahubiria
waumini wao ni kiongozi yupi na wa chama gani anafaa kuwa Rais wa awamu ya tano
wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania.
Jumuiya ya waislamu wa
Ahmadiya ilianzishwa machi 23,1889 huko nchini India na kwamba hadi sasa
jumuiya hiyo imefikisha umri wa miaka 126 ikiwa na wafuasi milioni 200 kwenye
nchi takribani 206 kote ulimwenguni.
Mwisho.
Waumini wa Jumuiya ya Ahmadiya Mjini Masasi wakifuatilia kwa ukaribu mada mbalimbali zilizokuwa zikiwakilishwa na walimu wa jumuiya hiyo kutoka maeneo mbalimbali ya mikoa ya Kanda ya Kusini. |
Baadhi ya viongozi na walimu mbalimbali wa Jumuiya ya Ahmadiya wakifuatilia mada mbalimbali kutoka kwa viongozi wa juu wa jumuiya hiyo.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD