TANGAZO
Na Clarence
Chilumba,Ruangwa.
JUMLA ya wananchi 82,795
ambao ni sawa na asilimia 99 katika wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi
wamejiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura kwa kutumia mfumo wa
kielektroniki wa BVR kwa ajili ya kushiriki kwenye uchaguzi mkuu pamoja na
kuipigia kura ya ndio au hapana katiba inayopendekezwa.
Akitoa taarifa jana ya
zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura kwa baraza la madiwani
la Halmashauri ya wilaya ya Ruangwa mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Nicholaus
Kombe alisema Halmashauri ya wilaya ya Ruangwa yenye jimbo moja la uchaguzi la
Ruangwa lilianza zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura April
24 mwaka huu na kumalizika Mei 25.
Alisema zoezi hilo wilayani humo lilidumu kwa
muda wa siku 28 za kazi ukiondoa siku za kuhamisha maofisa waandikishaji na
wataalamu wa BVR pamoja na vifaa toka kanda moja kwenda kanda zingine
zilizotengwa ndani ya jimbo hilo la uchaguzi.
Alisema uandikishaji
ulifanyika ndani ya siku saba katika kila kanda kama ilivyoelekezwa na tume ya
Taifa ya uchaguzi ambapo wilaya hiyo ilikuwa na kanda nne za uandikishaji
zilizokuwa na jumla ya vituo 182 vya uandikishaji.
Kwa mujibu wa Kombe
alisema lengo la uandikishaji katika Halmashauri ya wilaya ya Ruangwa lilikuwa
ni kuandikisha watu 83,672 kwa mujibu wa sensa ya ofisi ya takwimu ya Taifa (National
Bureau of Statistics-NBS 2015) ambapo watu walioandikishwa ni ni 82,795 sawa na
asilimia 99.
Alisema kutokana na
takwimu hizo ni dhahiri kuwa zoezi hilo la uandikishaji wilayani humo limevuka
lengo ambapo hakusita kuwapongeza madiwani pamoja na viongozi wote wa serikali
na vyama vya siasa ambao katika kipindi chote walitoa ushirikiano sambamba na
kutoa elimu kwa wananchi umuhimu wa kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la
wapiga kura.
Akizungumzia kuhusu
ushiriki wa vyama vya siasa katika zoezi hilo mkurugenzi huyo alisema kila
chama cha siasa chenye usajili wa kudumu kiliruhusiwa kuweka wakala mmoja kwa
kila kituo kwa mujibu wa sheria za uchaguzi ambao kwa kushirikiana na waandishi
wasaidizi wa vituo walifanya kazi ya kutambua wakazi na kutoa taarifa juu ya
watu wasio na sifa ya kuandikishwa.
Alisema kwa ujumla zoezi
hilo lilienda vizuri licha ya kuwepo kwa changamoto mbalimbali ambazo kwa
kushirikiana na wataalamu kutoka tume ya Taifa ya uchaguzi walifanikiwa
kufanikisha mchakato huo muhimu kwa watanzania hasa katika kipindi hiki
kuelekea kwenye uchaguzi mkuu wa Rais,wabunge na madiwani.
Mwisho.
TANGAZO
Facebook Blogger Plugin by WAYEGE CO.LTD